Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, mchana huu ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mama Anna Kilango Malecella, kwa kubaini kuwa alimwambia uwongo kuwa Mkoa wake hauna wafanyakazi hewa wakati kumbe wapo wengi tu.
 
Rais Magufuli amesema kwamba hakuamini kwamba kuna mkoa ambao hauna wafanyakazi hewa, hivyo akatuma kikosi kazi ambacho hadi usiku wa kuamkia leo kimebaini kuweko na wafanyakazi hewa 45 mkoani Shinyanya.
 
Rais Magufuli, ambaye alikuwa anaongea baada ya kupokea Ripoti ya TAKUKURU toka kwa Mkurugenzi wake Mkuu Valentino Mlowola, amesema kasikitishwa sana na kauli ya Mama Malecela ambaye bila shaka alikuwa amepata ushauri mbaya toka kwa watendaji wake.
 
Amesema idadi hiyo ya wafanyakazi hewa mkoani Shinyanga huenda ikaongezeka zaidi kwani wilaya mbili zilikuwa bado zinaendela kuhakikiwa.
 
Rais Magufuli amesema pia kwamba hadi jana jumla ya wafanyakazi hewa zaidi ya 5, 507 wamebainika nchi nzima, wengi wao wakitoka katika halmashauri.
 
Hivyo Rais pia ametengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Abdul R. Dachi kwa kumshauri vibaya Mkuu wa Mkoa.
 
Mama Anna Kilango Malecela, ambaye katika awamu ya nne alikuwa Naibu waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi na Mbunge wa Same Mashairiki, anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kwanza kuachishwa kazi. Wakuu wa mikoa waliapishwa mwezi uliopita.

Katika siku hiyo Rais aliwapa wakurugenzi wa halmashauri siku 15 wawatoe katika Orodha ya Malipo ya Mshahara (Pay Roll) wafanyakazi hewa wote katika halmashauri zote nchini, na kuwataka wakuu wa Mikoa hao wasimamie zoezi hilo kwa ukamilifu.
 
Vile vile Rais Magufuli alionya kuwa halmashauri yoyote baada ya muda huo itakayokuwa na mfanyakazi hewa, mkurugenzi wake atakuwa amejifuta kazi mwenyewe.Vilevile Rais amewaagiza mawaziri wote kuwaeleza watendaji wao wawaondoe wafanyakazi hewa wote ndani ya kipindi hicho cha siku 15 na kubainisha kuwa watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo watafukuzwa kazi kwani sheria ni msumeno.

0 comments:

Post a Comment

 
Top