Wakuu wa wilaya za Newala na Tambahimba mkoani Mtwara na wakurugenzi wa wilaya hizo kwa pamoja wamesema ununuzi wa kutumia kangomba katika mazao ya biashara hasa katika zao la korosho haukubaliki na wamejipanga kupambana nayo.
Hayo yalielezwa hapo jana katika kikao chao na viongozi wa chama kikuu cha ushirika cha Tandahimba Newala TANECU LIMITED kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Newala mjini humo.
Katika kikao hicho kiliichoitishwa na Mkuu wa wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo kwa upande wake ametaja sababu za kikao hicho kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wakulima kuhusu utendaji wa taasisi hiyo na mipango waliyonayo ya kuisaidia jamii wanayoihudumia.
MKUU WA WILAYA YA NEWALA MH. AZIZA MANGOSONGO
‘’Kwa taarifa nilizonazo nyie TANECU ni wababe wa vyama vya msingi na unaingilia mpaka mambo yao ya ndani hivyo nataka kujua sababu za kufanya hivyo ni zipi?.’’ Alihoji Mkuu huyo.
Aidha Bi. Aziza alihoji juu ya kuendelea kuwepo kwa biashara ya kangomba huku taasisi hiyo ikiwepo na ni mtetezini wa wakulima?
‘’Ninachoweza kusema hii ni dhuluma kwa wakulima hivyo katika msimu wa mwaka huu nataka kuona hakuna biashara ya kangomba na nitashinda huko huko vijijini na huyo atayejaribu lazima ashughulikiwe mapema’’. Aliongeza Mangosongo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Bw. Sebastian Waryoba amesma ni lazima kuwe na sheria zitakazo wabana wanunuzi kwa lengo la kuwaondoa wanunuzi wasio na uhakika wanaoyumbisha wakulima na kuwanyonya maslahi yao.
‘’Ni lazima kuwe na sheria za kuwabana wanunuzi bila hivyo haina maana ya kuwa na minada ya mauzo kwani mnada maana yake ni kuafikiana bei na pale mnunuzi anapokubali bei Fulani ni lazima afanye malipo na sio kum’bembeleza tena.’’ alisema Mkuu huyo wa wilaya.
MKUU WA WILAYA YA TANDAHIMBA MH. SEBASTIAN WARYOBA
Waryoba aliyazungumza hayo kufuatia maelezo ya kuwepo kwa changamoto ya wanunuzi wa korosho kuafiki bei kwenye mnada lakini kuchelewesha malipo au kugomea kabisa kulipa kwa sababu wanazozijua wao.
Nao Wakurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Newala Bw. Frank Mgaya na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae wamesema watahakikisha sheria ndogo ndogo zinatungwa katika vijiji na mitaa yao na kuzisimamia ili kudhibibiti upotevu wa mapato ambayo ndiyo chanzo cha maendeleo katika halmashauri zao.
‘’Ujue sisi halmashauri zetu zinategemea sana kodi zinazotokana na tozo za ushuru mbalimbali ndani ya vyanzo vyetu na hiki ni chanzo kimojawapo hivyo hatutakuwa tayari kuona wachache wananufaika na sisi tukakosa maendeleo.’’ Alisema Mkurungenzi wa halmashauri ya Mji wa Newala Frank Mgaya.
Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Newala Mussa Chimae alisema ‘’tena sio chanzo tu mapato bali ndio zao kuu la kiuchumi hivyo ni lazima wote tushirikiane kuwapa maendeleo wananchi kwani sote tunakazi moja tu ya kuwatumikia wananchi.’’
Meneja wa TANECU Bw. Hassan Chipyangu ilikiri kuwepo kwa malalamiko ya wakulima dhidi yao lakini hiyo inatokana na uelewa mdogo wa wakulima kuhusu majukumu na shughuli wanazozitekeleza.
Amesma wao wanasimamia kutoa mwongozo kwa vyama vya msingi na TANECU haiusiki moja kwa moja katika kusimamia shughuli zao na mambo yakifedha.
Hata hivyo alisema TANECU ipo tayari kushirikiana na serikali kukomesha biashara ya kangomba kwani hata baadhi ya wahusika wanawatambua huku akiusifu uongozi huo kwa hatua waliyoichukua ya kuwaita na kukaa meza moja kwani haijawahi tokea hapo awali kwa viongozi waliopita.
0 comments:
Post a Comment