Uongozi wa wakulima wa bonde la Chihanga katika Mradi wa Lipeleng’enye ulilopo kata ya Mkunya Tarafa ya Mkunya wilayani Newala umepewa siku 21 kuhakikisha wakuliwa wote katika eneo hilo wamelima maeneo yao. 
Agizo hilo limetolewa na Afisa Tarafa wa Mkunya Bw. Paul Simwela katika kikao chake na wakulima pamoja na viongozi wa mradi huo kilichofanyika Jumatano July 27 Mwaka huu, kijijini Chihanga kwa lengo la kujadili maendeleo na changamoto zilizopo katika mradi huo. 

Baadhi ya Wakulima hao Said Almani, Chaku Shaibu Kalenje na Viongozi wa Mradi huo kwa pamoja walisema hali ya kilimo katika bonge hilo kwa sasa hairidhishi kwa kuwa uzalishaji umeshuka na siku hadi siku unapungua zaidi na hiyo inatokana na baadhi ya wakuliwa kushikilia maeneo huku wakiwa hawako tayari kufanya shughuli za kilimo. 

“Kutokana na bonde hili upo uwezekanao wa umaskini tuliokuwa nao tunauvua kama koti na tunautupa huko lakini kinachotakiwa kwa sasa serikali inatakiwa iote meno ili kupunuza baadhi ya matatizo yaliyopo.” alieleza Said Almani. 
Kwa upande wake Chaku Shaibu aliongeza kwa kusema kuwa “serikali ndio kila kitu sasa haitakiwa kufumbia macho mambo kama haya yanayojitokeza na zaidi iwachukulie hatua vijana kwa viongozi kuacha kuwanunulia bodaboda badala yake kuwahimiza kufanya shughuli za kilimo.” 


Muonekano wa Bonde la Mto Ruvuma kutoka Newala (Picha kwa Masaada wa Mtandao) 

Afisa Mtendaji mtendaji wa kijiji cha Chihanga Bw. Bashilu Musa Namawe ambaye pia ni mkulima katika bonde hilo, amesema pamoja na wakulima kutokufanya kazi lakini changamoto kubwa iliyopo ni ubovu wa miundombinu ambapo mifereji ya kupitishia maji imejaa mchanga na wahusika wa maeneo hawawajibiki kusafisha kwa kuondoa mchanga huo, na baadhi ya maeneo yamekuwa na maji mengi kwa kipindi chote cha mwaka. 

Kufuatia maelezo hayo Afisa huyo aliuagiza uongozi wa wakulima hao kuandaa majina ya wakulima watakaoshindwa kuyafanyia kazi maeneo yao ndani ya siku hizo 21 ili yachukuliwe na kupatiwa watu wengine wenye nia ya kuyafanyia kazi. 

AFISA TARAFA YA MKUNYA PAUL SIMWELA 

“Haiwezekani Newala tunakosa mbogamboga mpaka tuagize toka mbali wakati sisi wenyewe tunaouwezo wa kuzalisha na maeneo tunayo, sasa ndani ya siku hizo 21 asiyefanyia kazi eneo lake leteni orodha yao, ili hayo maeneo wapatiwe watu wenye nia ya kufanyakazi na wapo wengi, pamoja na vijana wanaodhurula, kukaa vijiweni wakicheza karata na pool lazima tuwakamate waje kufanyakazi kama agizo la Rais lilivyo la kuwataka watu wote wafanyekazi.” Alisema Simwela. 

Aidha Simwela alisema serikali kupitia halmashauri na wafadhili mbalimbali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuwekeza katika bonde hilo hivyo yeye kama kiongozi wa eneo hilo hayupo tayari kuona fedha hizo zinapotea bila manufaa kwa jamii na lazima hatua zichukuliwe kuanzia chini. 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Mkunya Frank Msuya amewataka wakulima hao kutumia fursa ya bonde hilo kujiongezea kipato kwa kuzalisha mazao ya biashara sambamba na kuwatumia wataalam mbalimbali wa kilimo kikamilifu ambao wanalipwa kupitia kodi zao. 

Kwa mujibu wa Afisa Tarafa huyo amefahamisha kuwa mradi wa Lipeleng’enye unaosimamiwa na Idara ya Kilimo ya halmashauri ya wilaya ya Newala, na kusaidiwa na wafadhili mbalimbali wakiwamo JICA na AGHAKAN ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2008/2009 mpaka sasa umetumia shilingi bilioni moja milioni mia moja na tisini (Tsh. 1,190,000,000/=) kurekebisha minundo mbinu yake. 




0 comments:

Post a Comment

 
Top